Benki
ya CRDB imetajwa miongoni mwa taasisi salama zaidi za fedha duniani,
hivyo kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi 11 kutoka Afrika zilizokidhi
vigezo hivyo.
Utafiti
uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Globa Finance ulihusisha nchi 106
na taasisi husika zikawekwa kwenye makundi ya benki 50 salama zaidi
duniani, benki 50 za biashara salama zaidi duniani, benki 50 salama
zaidi kutoka nchi zinazoibukia kiuchumi, benki salama zaidi ya Kiislamu
na benki bora kwa kanda ya Afrika, Asia, Ulaya, Mashariki ya Mbali na
Amerika.
Kukidhi vigezo na kuwemo kwenye orodha hiyo, Benki 1,000 kubwa zaidi zilifanyiwa tathmini kwa kuzingatia vigezo tofauti.
Mkurugenzi
wa idara ya habari wa Global Finance, Joseph Giarraputo amesema
kulikuwa na changamoto wakati wa kukamilisha mchakato huo na hasa kwa
benki zenye matawi kwenye zaidi ya nchi moja na zinahudumia wateja wenye
ofisi katika mataifa tofauti.
“Licha
ya juhudi tulizozifanya kuzihuisha, kanuni za uendeshaji wa benki
zimekuwa tofauti kwa kila nchi kutokana na changamoto zilizopo pamoja na
rasilimali,” amesema Giarraputo.
Mkurugenzi
wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa CRDB, Tully Mwambapa amesema
ushirikiano wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ndiyo chachu ya mafanikio
ndani na nje ya mipaka.
“Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa huduma bora kwa mteja. Usalama wa taarifa za wateja wetu ni kitu kinachopewa kipaumbele.
Hii ni kwa maeneo yote; mikopo, huduma za mtandaoni hata kwa simu za mkononi,” amesema Mwambapa.
Licha ya CRDB yenye thamani ya Sh5.49 trilioni, taasisi tatu kutoka kaskazini mwa Afrika nazo zimetajwa.
Hizi ni National Bank of Egypt (Misri), Attijariwafa Bank ya Morocco na Arab Tunisian Bank ya Tunisia.
Kutoka
Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuna Banco Angolano de Investimentos ya
Angola, Rawbank ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Standard Bank
ya Afrika Kusini, GCB ya Ghana, Zenith ya Nigeria, Ecobank ya Togo na
Stanbic ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment