BENKI ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB), imeelezea kuridhishwa na kasi pamoja na viwango vya miradi ya
ujenzi ya barabara inayofadhiliwa na benki hiyo katika Ukanda wa Kusini, na
kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuchochea
ukuaji wa uchumi wa Taifa na wananchi wake.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo anayesimamia Kanda wa Afrika Mashariki, Dkt.
Nyamajeje Weggoro, baada ya kutembelea na kukagua barabara ya
Tunduru-Nangaka-Mtambaswala, mkoani Mtwara, yenye urefu wa kilometa 202.2.
Barabara hiyo yenye
vipande vitatu imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 180 kupitia ufadhili
wa benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) na
Serikali ya Tanzania.
Dkt. Weggoro amesema kuwa
barabara hiyo ambayo upande mmoja inaunganisha Tanzania na Msumbiji, itachochea
maendeleo ya wananchi kutoka pande hizo mbili kwa kusafirisha watu na bidhaa
kwa urahisi zaidi.
“Nimeona mabadiliko
makubwa sana, si tu kwa barabara, lakini maisha ya watu, mabadiliko ambayo ni
dhahiri yanatokana na hii miradi ya barabara ambayo imefungua fursa nyingi za
maendeleo, watu wanafanyabiashara lakini pia wanatembeleana!” alisema Dkt.
Weggoro.
Alitoa wito kwa
Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa barabara hizo kujiletea maendeleo kwa
kufanyabiashara hivyo kujikwamua kiuchumi.
Mhandisi Heldaus Jerome
kutoka Wakala wa Barabara -Tanroads, Makao Makuu, alisema kuwa barabara hiyo ya
Tunduru-Mangaka-Mtambaswala, ina vipande vitatu, kutoka Mangaka – Nakapanya (km
70.5), Nakapanya – Tunduru (66.5) na Mangaka – Mtambaswala (km 65.5)
Alifafanua kuwa gharama
za ujenzi wa mradi huo, kiasi cha Dola milioni 210, kimetolewa na AfDB
(64.79%), Shirika la Maendeleo la Japan-JICA (32.83%) na Serikali ya Tanzania
(2.38%) na kwamba Wadau hao pia wanafadhili ujenzi wa barabara kutoka
Dodoma-Babati yenye urefu wa kilometa 180.53.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Mangaka wilayani Masasi mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa uchumi na maisha yao kwa ujumla kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Mangaka wilayani Masasi mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo muhimu kwa uchumi na maisha yao kwa ujumla kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kilimanihewa, Bw. Abbas Muhidin Mwira, alisema kuwa maeneo ya Mangaka
yamechangamka kibiashara na vijana wengi wamejiajiri wenyewe kwa
kufanyabiashara zinazowaingizia kipato huku huduma za usafiri zikiboreshwa
baada ya mabasi ya abiria yaendayo mikoani pamoja na malori yanayobeba saruji
kutoka Kiwanda cha Saruji cha Dangote-Mtwara kuanza kupita njia hiyo na
kusisimua biashara zao.
0 comments:
Post a Comment