Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani (kushoto), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo wakifungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa kiwanda cha Inhemeter kinachojishughulisha na kutengeneza vifaa vya kuunganishia mifumo ya umeme kutoka katika miundombinu mikubwa na kupeleka majumbani hafla hiyo imefanyika jana kiwandani hapo kinondoni Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akizungumza na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wafanyakazi wa kampuni ya Inhemeter wakati akizindua kiwanda cha Inhemeter kinachojishughulisha na kutengeneza vifaa vya kuunganishia mifumo ya umeme kutoka katika miundombinu mikubwa na kupeleka majumbani yaani kwa wananchi hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mh Daniel Chongolo. Hafla hiyo imefanyika jana jjini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Inhemeter , Abraham Rajakili akizungumza wakati wa hafla hiyo
Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Inhemeter , Abraham Rajakili wakati alipotembelea kiwanda hicho na kukizindua rasmi.WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani amesema kuwa Serikali haitaruhusu tena uingizwaji wa vifaa mbalimbali vya kuunganishia umeme kutoka nje ya nchi kwa sababu tayari hapa nchini kuna viwanda vya kutosha vya kuzalisha vifaa hivyo.
Pia Dk. Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Umeme Vijiji (REA) na wakandarasi wanaochukua tenda za kusambaza umeme vijijini kuacha kuagiza vifaa nje ya nchi badala yake kuchukua vya ndani ili kuweza kupunguza gharama na kuokoa muda wa kupeleka umeme kwa wananchi.
Dk. Kalemani ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kiwanda cha Inhemeter kinachojishughulisha na kutengeneza vifaa vya kuunganishia mifumo ya umeme kutoka katika miundombinu mikubwa na kupeleka majumbani yaani kwa wananchi.
Amesema hakuna kifaa chochote cha kuunganisha umeme kitakachotoka nje ya nchi kwa sasa na kuongeza kuwa manunuzi yote ya vifaa mbalimbali vya umeme ikiwamo nguzo na trasnfoma vinunuliwe hapa nchini.
"Umeme ni muhimu sana katika maendeleo na uchumi wa viwanda na kamwe uwezi kusema unataka kujenga uchumi wa viwanda alafu unategemea vifaa kutoka nje ya nchi hivyo Serikali itaendelea kusisitiza watu kununua vifaa vinavyotengenezwa hapa nchini na ujengwaji wa viwanda vya ndani," amesema
Aidha amesema hadi kufikia leo Julai 10, 2020 jumla ya vijiji 9512 vimeshasambaziwa umeme huku vijiji 2700 vilivyobakiwa vikiratajia kuanza kuwekewa umeme Agosti mwaka huu.
Dk. Kalemani amesema kuanzia Agosti 20 hadi Septemba 20 mwaka huu, Serikali itaanza kusambaza wakandarasi watakaofanya kazi ya kuvipelekea umeme vijiji na vitongoji vyote vilivyosalia kupata umeme hapa nchini.
Amesema takribani kiasi cha Sh. Bilioni 851 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo na kuongeza kuwa anakipongeza kiwanda cha Inhemeter kwa uzalishaji wa viunganishi zaidi ya 600,000 vya umeme kutoka miundombinu mikubwa kwenda kwa wananchi huku mahitaji ya nani ya vifaa hivyo yakiwa 300,000.
"Pamoja na kwamba mtazalisha vifaa vingi hakikisheni mnazingatia viwango na ubora unaokubalika ili viweze kuuzika hapa nchini na nje ya nchi," amesema Dk Kalemani.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Abraham Rajakili amesema uwekezaji katika kiwanda hicho unathamani ya Shilingi Bilioni tano na kusisitiza kuwa bidhaa zina ubora na viwango vinavyokubalika.
Amesema kwa sasa wauwezo wa kuzalisha vifaa hivyo vya kuunganishia umeme vipatavyo Milioni 1.5 kwa mwaka na wanategemea kutoa ajira 120 katika kiwanda hicho huku aliongeza kusema kuwa idadi hiyo ya ajira itaongezeka kutokana na ongezeko la uzalishaji.
"Lengo letu si tu kuzalisha bidhaa hizi hapa Tanzania tu bali kuziuza nje ya nchi hivyo tunahitaji kupata ushirikiano kutoka kwa Serikali ili jambo hili liweze kutimia," amesema
0 comments:
Post a Comment