Katika hatua muhimu ya kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa jamii za wenyeji na mazingira, Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) na WWF Tanzania wamekabidhi rasmi miundombinu ya mfumo wa maji unaotumia nishati ya jua, ikijumuisha kisima, sehemu ya kunyweshea mifugo, na kituo cha maji kwa matumizi ya nyumbani katika Wilaya ya Kibaha.
Katika tukio hilo hilo, washirika hao wawili pia walizindua mradi wa majaribio wa miradi ya urejeshaji wa mazingira chini ya mpango wa "Bankable Nature Solutions" (BNbS) ili kuimarisha usalama wa maji wa muda mrefu na ulinzi wa mazingira.
Hafla ya makabidhiano iliyofanyika Kijiji cha Minazimikinda, Wilaya ya Kibaha, ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Nickson Simon John, ambaye alisifu ushirikiano kati ya TBL na WWF. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za maji nchini, hususan katika maeneo yanayokua kwa kasi kama Pwani na Dar es Salaam.
"Maji ni rasilimali muhimu kwa ukuaji wa jamii zetu na uchumi. Ushirikiano huu unaonesha nguvu ya kufanya kazi kwa pamoja katika kutatua uhaba wa maji. Juhudi za TBL na WWF Tanzania za kuboresha usalama wa maji, hasa katika Dar es Salaam na maeneo jirani, ni za kupongezwa na ni hatua muhimu kuelekea kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi kwa wote," alisema Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Nickson Simon John.
Mfumo mpya wa maji unaotumia nishati ya jua utatoa maji safi na ya kuaminika kwa jamii zinazozunguka, ukiwasaidia kaya na mifugo katika eneo hilo. Miundombinu hii inashughulikia changamoto za uhaba wa maji kwa sasa na kutumia teknolojia rafiki wa mazingira ili kuhakikisha matumizi endelevu kwa muda mrefu.
Mradi huu ni sehemu ya dhamira kubwa ya TBL kwa uendelevu, inayooana na mkakati wake wa kuleta athari chanya kwa jamii inazozihudumia huku ikiunga mkono uhifadhi wa rasilimali za asili za Tanzania. Ushirikiano na WWF Tanzania chini ya mpango wa BNbS unalenga kuhakikisha kuwa mifumo ya asili inabaki salama wakati changamoto za maji zinashughulikiwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Michelle Kilpin, alisisitiza umuhimu wa mradi huo: "Kwa TBL, uendelevu ni msingi wa shughuli zetu. Mfumo huu wa maji unaotumia nishati ya jua, pamoja na uzinduzi wa mradi wa majaribio wa Bankable Nature Solutions, ni hatua muhimu kuelekea kuhakikisha kwamba watu na mazingira wote wananufaika na juhudi zetu. Kwa kushirikiana kwa karibu na WWF Tanzania, tunahakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii hii na kulinda mifumo muhimu ya ikolojia ambayo ni muhimu kwa mustakabali wetu."
Mbinu ya Bankable Nature Solutions (BNbS) inatumia rasilimali za asili kwa njia endelevu, ikigeuza juhudi za uhifadhi wa mazingira kuwa miradi inayoweza kujiendesha kifedha na kuleta manufaa kwa uchumi na jamii. Kupitia mpango huu, TBL na WWF Tanzania wanalenga kuunda mfano wa kurudiwa unaoweza kutekelezwa nchi nzima ili kukabiliana na uhaba wa maji na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Mkurugenzi wa Nchi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru, alielezea umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji. “Ulinzi wa vyanzo muhimu vya maji ni muhimu kwa kudumisha maisha ya binadamu na usawa wa mazingira. Kupitia mbinu za ubunifu kama Bankable Nature Solutions, tunaweza kuunda suluhisho la muda mrefu kwa ajili ya watu na mazingira.”
"Ushirikiano wetu na TBL unaonesha jinsi biashara na mashirika ya uhifadhi wa mazingira yanavyoweza kushirikiana kufanikisha matokeo ya kudumu. Kwa uzinduzi wa mradi wa majaribio wa BNbS hapa Kibaha, tunaweka msingi wa suluhisho za muda mrefu na endelevu ambazo zinalinda rasilimali zetu za asili huku zikihakikisha jamii zinapata huduma muhimu kama maji." alisema Dkt. Ngusaru
Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo, wanajamii, na wadau muhimu ambao walipongeza mpango huo kwa kuwa na mtazamo wa mbali na manufaa ya muda mrefu kwa jamii. Kisima cha maji cha nishati ya jua, sehemu ya kunyweshea mifugo, na kituo cha maji kwa matumizi ya nyumbani vinatarajiwa kunufaisha moja kwa moja mamia ya kaya na mifugo yao.
Ushirikiano kati ya TBL na WWF Tanzania haukabiliani tu na upungufu wa maji, bali pia unaimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji, muhimu kwa kuhifadhi bioanuwai na kudumisha huduma za mazingira kwa vizazi vijavyo.
0 comments:
Post a Comment