Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Lilian Swere (wa pili kushoto) akionyesha jina la mshindi wa droo ya kwanza ya kampeni ya Tumia na Ushinde 'Spend & Win' ambapo mkazi wa Dar es Salaam Bw, Rashid Nassoro Said aliibuka kidedea kwa kujishindia gari jipya aina ya Subaru Forester 2024 lenye thamani ya zaidi ya shs milioni 40. Kampeni hiyo inayochezeshwa kila mwezi kwa kwa muda wa miezi mitatu, inahamasisha matumizi ya kadi na hduma za kidigitali katika kufanya miamala mbalimbali ya kibenki. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.
Benki ya Absa Tanzania imesema imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi na kwa gharama nafuu.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Lilian Swere wakati wa droo ya kwanza ya Kampeni ianyoendelea ya ‘Tumia Ushinde’ (Spend & Win), ambayo lengo lake kubwa ni kuhamasisha wateja wa benki hiyo na watanzania kufanya miamala mbalimbali ya kibenki kwa kutumia kadi ama huduma za kibenki kwa njia za kidigitali.
“Kampeni hii ya miezi mitatu ina lengo la kuwazawadia gari wateja wetu wanaofanya miamala ya kibenki kwa kutumia kadi za ATM ama huduma za kidigitali kwa kutumia mifumo yetu inayowawezesha wateja kupata huduma kiuharaka na kiurahisi hivyo kutimiza malengo yao."
“Sisi kama Absa Benki Tanzania tumeimarisha huduma zetu za kidigitali ili kwenda sambamba na jitihada zinazofanywa na serikali kusaidia kufikisha huduma za kibenki kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hizi huku wakiendelea kutumia mifumo ya kibenki ya kiasili."
“Mifumo ya kidigitali ya benki yetu ni ya haraka na tumeimarisha kwa kiwango cha kimataifa mifumo ya usalama hivyo tunapenda kuwatoa hofu wateja wetu wote kuendelea kufanya miamala kwa kutumia mifumo yetu ya kidigitali bila hofu yoyote”, alisema Bi. Ndabu.
Naye Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Aron Luhanga alisema kampeni hiyo inaenda sambamba na lengo kuu la kuwepo kwa benki hiyo ambalo ni kuiwezesha Afrika na Tanzania ya Kesho, hatua moja baada ya nyingine ikiwezeshwa na chapa mpya ya benki hiyo isemayo ‘Stori yako ni ya thamani’.
“Tunapotoa zawadi hii kwa wateja wetu na huku tukiboresha huduma zetu kwa njia za kidigitali tunaamini kuwa tunasaidia kuandika stori mbalimbali za washindi na wateja wetu, lakini pia tunaisaidia serikali yetu kuandika stori yake ya kuona huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi kila kona ya nchi yetu”, alisema Bw. Luhanga.
Kampeni ya Spend & Win itadumu kwa muda wa miezi mitatu na ikishuhudia kila mwezi mshindi mmoja akiibuka na gari jipya aina ya Subaru Forester lenye thamani za zaidi sh shs milioni 40, ambapo mshindi hutakiwa kufanya miamala kila wakati kwa kutumia kadi ama huduma za kibenki kwa njia ya mtandao. Katika hafla ya jana, mkazi wa Dar es Salaam, Rashidi Nassoro Saidi aliibuka kidedea na kujishindia moja ya zawadi hiyo ya gari.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Aron Luhanga (kulia) akizungumzai jijini Dar es Salaam jana wakati wa droo ya kwanza ya kampeni ya Tumia na Ushinde 'Spend & Win' ambapo mkazi wa Dar es Salaam Bw, Rashid Nassoro Said aliibuka kidedea kwa kujishindia gari jipya aina ya Subaru Forester 2024 lenye thamani ya zaidi ya shs milioni 40. Kampeni hiyo inayochezeshwa kila mwezi kwa kwa muda wa miezi mitatu, inahamasisha matumizi ya kadi na huduma za kidigitali katika kufanya miamala mbalimbali ya kibenki. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.
0 comments:
Post a Comment