Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC,Peter Nalitolela akizungumza katika kongamano la siku moja kuhusu mitaji ya fedha na usimamizi wa hatari zinazoweza kutokea katika miamala ya kifedha kwa wadau kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania, Tanesco, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kongamano hilo lilifanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imesema itaendelea kushirikiana kikamilifu na serikali ya awamu ya tano katika azma yake ya kuwaletea wananchi wake uchumi wa kweli na maendeleo imeelezwa jijini Dodoma mwisho mwa wiki.
Akizungumza wakati wa kongamano la wadau juu ya upatikaji wa fedha na usimamizi wa hatari zinazoweza kujitokeza katika miamala ya kifedha lililoandaliwa kwa wadau, Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko wa NBC, Peter Nalitolela alisema NBC imejizatiti kushirikiana na serikali na taasisi zake katika kuhakikisha nchi inafaidika na kiasi cha pesa inachotumia katika miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo inayoendelea kufanyika.
Alisema kongamano hilo lililohudhuriwa na wadau kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tanesco, TPDC na Wizara ya Fedha na Mipango lilikuwa na lengo kubwa ya kuangalia vyanzo mbalimbali vya fedha vinavyopatikana katika miradi mbalimbali mikubwa inayofanywa na serikali pamoja na kuangalia usimamizi wa hatari katika miamala ya kifedha inayoweza kutokea katika miradi hiyo.
“Kama mjuavyo miradi mbalimbali mikubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano kama vile mradi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge, ujenzi wa barabara na madaraja, baadhi ya miradi hufanywa kwa mikopo kutoka pande tofauti, hivyo tulitaka kuonyesha uwezo wetu kama NBC katika kusaidia upatikanaji wa fedha na pia linapokuja suala la uzimamizi wa hatari za kifedha katika miamala hiyo.
“Kilicho kikubwa ni kwa NBC kuangalia uwezo wetu kwa njia tofauti tofauti ikiwemo katika kukopesha, lakini pia kuona serikali haipati hasara kutokana na masuala ya riba, fedha za kigeni na kushuka kwa thamani ya shilingi, hivyo NBC tumejiandaa kushirikiana na serikali kikamilifu katika kutimiza azma yake, kwa uwezo wetu tunaweza kushirikiana zaidi na zaidi”, aliongeza Bwana Nalitolela.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo alisema kama inavyofahamika kuwa NBC inamilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Benki ya Absa ya Afrika Kusini pamoja na Benki ya Dunia,hii huiweka NBC katika nafasi nzuri ya kusaidia juhudi za serikali.
Katika kongamano hilo pia NBC Ilileta wataalam kutoka benki mama ya Absa ili kuweza kuonyesha uzoefu wao walioupata kupitia miamala waliyofanya na serikali za nchi mbalimbali barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment