Meneja Mawasiliano wa Bodi yaUtaliiTanzania(TTB), hiyo Paulina Mkama (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upigaji kura wa tuzo za kimataifa zinazotambua na kuthamini ubora, ubunifu na huduma bora katika sekta ya utalii na usafiri duniani. (Katikati), ni Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru pamoja na Meneja Masoko wa wa bodi hiyo Vivian Temi
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeingia kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo za Dunia za Utalii ( World Travel Award 2025) baada ya kuteuliwa kushiriki katika vipengele 20 vyenye wagombea 24 vikiwemo taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii.
Akizungumza Oktoba 13, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upigaji kura, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwani inaonyesha jinsi Tanzania inavyozidi kutambulika kimataifa.
“Kwa kawaida Tanzania imekuwa ikishinda katika tuzo za ngazi ya Afrika , lakini mwaka huu tumeingia katika mashindano ya dunia, mwaka jana tulichaguliwa kama nchi bora kwa safari za utalii, jambo ambalo limeendelea kuitangaza nchi yetu zaidi,” amesema Mafuru.
Ameeleza kuwa World Travel Award( WTA) ni tuzo za kimataifa zinazotambua na kuthamini ubora, ubunifu na huduma bora katika sekta ya utalii na usafiri duniani.
“Tuzo hizi zilianzishwa mwaka 1993, na kwa sasa zinajulikana kama, Oscars za sekta za Utalii , kutokana na heshima na ushawishi wake katika kuonyesha viwango vya juu vya ubora duniani,” amefafanua Mafuru.
Mafuru amesema lengo la tuzo hizo ni kutambua na kuhamasisha ubora katika nyanja zote za utalii, ikiwemo mashirika ya ndege, hifadhi za taifa, hoteli, miji ya kitalii, kampuni za usafiri na taasisi za utalii za kitaifa kama TTB.
Amewahamasisha watanzania wote kujitokeza kupiga kura kupitia simu zao na mitandao ya kijamii katika kampeni iliyoanza oktoba 6 hadi oktoba 16,2025 , ili Tanzania iweze kushinda katika vipengele mbalimbali ikiwemo Nchi bora ya Utalii, Bodi Bora ya Utalii, Hifadhi Bora, Kivutio Bora na Uwanja bora wa ndege.
“Ushindi katika tuzo hizi utaongeza hadhi ya Tanzania katika sekta ya utalii duniani, kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha juhudi za kulinda rasilimali na urithi wa taifa,” amesema .
Aidha, Mafuru amesisitiza kuwa mafanikio yanayoonekana sasa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara katika kutangaza vivutio vya utalii kupitia ziara na filamu ya Royal Tour pamoja na hotuba zake
0 comments:
Post a Comment