KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania yamkosha Naibu Waziri wa Nishati yakabidhi mitungi na majiko yake 1000 kwa washiriki wa mashindano ya kupika kwa gesi ya Oryx mkoani Mbeya ili kuwawezesha kurahisisha shughuli zao za mapishi.
Akizungumza wakati akihitimisha mashindano ya kupika kutumia Nishati ya ORYX kwa Mama na Baba Lishe wa Mkoa wa mbeya, Naibu Waziri Judith Kapinga aliyekuwa mgeni rasmi amesema Serikali imekuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na lengo ni kufika asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati mbadala kwaajili ya kupikia.
"Maombi ya wananchi kwa wadau wa gesi ni kupunguzwa kwa bei ya nishati hiyo ambayo kwa sasa ni ipo juu kulingana na kipato Cha wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa Nishati hiyo. Tunashauri wadau katika sekta hii kutengenezwe mfumo ambao utakuwa rafiki kwa Mwananchi kununua gesi kidogo kidogo pindi anapokuwa na uhitaji."
Amesisitiza kukiwa na uwezo wa gesi kununuliwa kidogo kidogo anaamini wananchi wengi watatumia gesi na hivyo kusaidia kupunguza Kasi ya uharibu wa mazingira lakini pia kulinda afya za wananchi.
Naibu Waziri Kapinga amesema katika mwaka wa fedha uliopita wamegawa mitungi kwa wananchi na mwaka huu wa fedha wametenga fedha kwa ajili ya kuendelea kugawa nishati mbadala ya kupikia kwa wananchi huku akisisitiza kuwa Rais DK.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuona asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia nishati hiyo.
Kuhusu mashindano hayo ya mapishi, Naibu Waziri Kapinga amempongeza Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson kuandaa mashindano hayo makubwa na kushirikisha Mama na Baba Lishe 1000 kushindana kupika kwa gesi kwani yamekuwa ya mfano na yametumika kutoa elimu ya nishati na utunzaji mazingira.
Naibu Waziri pia amewashukuru Oryx gas kwa kuendelea kuishika mkono Serikali katika kusaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, wanafanya kazi nzuri na wamekuwa wakifika kila mahali wakigawa mitungi na majiko yake kwa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema lengo kuu la mashindano ya mapishi ni kuhamasika matumizi ya nishati safi kwa lengo la kulinda mazingira ambayo yamekuwa yakiharibiwa kwasababu ya kukata kuni na mkaa.
"Kwa miaka zaidi ya 15 iliyopita upatikanaji wa nishati ya kupikia umekuwa ukipangwa na kujadiliwa lakini hivi sasa Serikali inayoongozwa na Rais DK.Samia Suluhu Hassan amekuwa na hamasa kubwa ya kuhimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia."
"Oryx Gasi tunaamini kupika kwa gesi kunakwenda kusaidia kulinda mazingira sambamba na kupunguza muda mwingi kwa wanawake kuwa porini kutafuta kuni na mkaa kwa ajili ya kuanda chakula.Pia kupika kwa gesi kutasaidia kuwalinda wanawake dhidi ya wanyama wakali walioko misitu lakini kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatilii ambavyo wanakutana navyo wakiwa porini."Amesema Benoit.
Ameongeza "pamoja na kusaidia makundi mbalimbali kuyawawezesha kupata mitungi ya gesi ya Oryx lakini wanajivunia kuwafikia Mama na Baba Lishe zaidi ya 12000 ambao wamepata elimu ya matumizi salama ya kupika kwa gesi sambamba na kuwapa mitungi midogo na mikubwa kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli za mapishi kwa urahisi na kuwa salama kiafya," amesema.
Kwa upande wao baadhi ya Mama na Baba Lishe walioshiriki mashindano ya kupika kwa gesi wamesema kupitia mashindano hayo wamenufaika na mafunzo waliyoyapata sambamba na kuelezwa umuhimu wa kutunza mazingira na wanatoa shukrani kwa waandaaji wakiongozwa na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dk.Tulia Ackson.
0 comments:
Post a Comment