Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko akikabidhi cheti cha shukurani kwa Meneja Rasilimali Watu wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport, Bi. Evalyn Hall (kulia), kutambua mchango wa kampuni hiyo kama mdhamini mkuu wa mbio za Rombo Marathon 2023 zilizotimua vumbi lake mjini Rombo mkoani Kilimanjaro jana. Kulia kwa Naibu waziri mkuu ni Waziri wa Elimu na Mbunge wa Rombo, Prof. Adolf Mkenda na kushoto kwake ni Waziri Biteko ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bwana Nurdin Babu.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport, Bwana Nderingo Materu (wa pili kushoto), Mkuu wa Mauzo wa kampuni hiyo, Bwana Lugano Kasambala (kushoto kwake), pamoja na wakimbiaji wengine, wakishiriki mbio za Rombo Marathon mjini Rombo, Kilimanjaro jana. Mbio hizo zilizodhaminiwa na Bayport, zina lengo la kuhamasisha vivutio vya utalii mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bwana Nurdin Babu (kulia), pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Kifedha ya Bayport, wakishiriki mbio za Rombo Marathon mjini Romb, Kilimanjaro jana. Mbio hizo zilizodhaminiwa na Bayport, zina lengo la kuhamasisha vivutio vya utalii mkoani humo.
Na mwandishi wetu, Rombo, Kilimanjaro
TAASISI ya Kifedha ya Bayport imenogesha na kufanikisha mbio za Rombo Marathon 2023 zilizofanyika mjini Rombo, Kilimanjaro jana, zikiwa na lengo la kuhamasisha vivutio vya utalii wilayani humo.
Ikiwa ni mwaka wa pili sasa Rombo Marathon imefanyika ikihudhuriwa na viongozi wa kiserikali, wageni, na watu mashuhuri huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dk. Doto Biteko.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Bayport, Bwana Nderingo Materu alisema Bayport ilikubali kuwa mdhamini Rombo Marathon ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali pamoja na muasisi wa mbio hizo, Waziri wa Elimu na Mbunge wa Rombo, Prof. Adolf Mkenda katika kukuza utalii pamoja na suala zima la uhifadhi wa mazingira.
“Kama mnavyofahamu sisi Bayport tumekuwa namba moja katika suala la utunzaji wa mazingira kwa njia ya upandaji miti, leo hii tumeamua kudhamini Rombo Marathon na tutaendelea kuunga mkono juhudi zozote nchini zenye lengo la kukuza utalii na kuhifadhi mazingira."
“Lakini pia kama inavyofahamika umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili kwa ajili ya ubora wa afya za wafanyakazi na familia zetu, tunaamini mbio hizi zitaleta hamasa pia kwa watanzania kutilia mkazo umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” alisema Bwana Materu.
Katika hotuba yake, Naibu Waziri Mkuu, Mhe, Dk. Biteko alitoa pongezi kwa waandaaji na wadhamini wa mbio za Rombo Marathon akisema zimekuwa na mafanikio makubwa lakini kikubwa ikiwa ni kujifunza utamaduni wa wana Rombo pamoja ya vivutio vya utalii vinavyopatikana katika wilaya na mkoa huo.
“Natoa pongezi nyingi kwa muasisi wa Rombo Marathon, Waziri wa Elimu na Mbunge wa Rombo, Prof. Mkenda, natoa pongezi kwa serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Rombo bila kuwasahau wadhamini wote waliojitolea rasilimali zao kufanikisha tukio hili."
“Serikali chini ya Rais, Mhe, Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono juhudi yoyote inayofanywa yenye lengo la kuwaletea maendeleo watu wa Rombo na kwa watanzania kwa ujumla,” alisema Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu.
Naye Waziri wa Elimu, Mbunge wa Rombo na muasisi wa mbio hizo, Prof. Adolf Mkenda alitoa shukurani zake kwa Mhe. Naibu Waziri Mkuu, Dk. Biteko kwa kukubali kuwa mgeni rasmi pamoja na wadhamini wa mbio hizo Taasisi ya Kifedha ya Bayport kwa kufanikisha tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya watu wa Rombo na wananchi wa Kilimanjaro.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kuungana na wana Rombo katika kushiriki tukio hili, natoa pia shukrani kwa wadhamini wote waliowezesha kufanya tukio hili kuwa lenye ubora ikiwemo Taasisi ya Bayport Financial Services,” alisema Prof. Mkenda.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bwana Nurdin Babu, alichukua nafasi hiyo kuwakaribisha wageni wote wanaotoka ndani na nje ya Tanzania kwenda kuangalia vivutio vya utalii mkoani humo akisema Kilimanjaro ipo salama na wapo tayari kuwapokea na kuwahudumia.
Mbio za Rombo Marathon zinazofanyika kwa mwaka wa pili sasa zimeshirikisha mbio za Km 21, Km 10 na mbio za kujifurahisa za kilomita 5.