Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Mhe. Paul Makonda ametembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi
wa Machinjio ya kisasa Vingunguti ikiwa ni mkakati wake wa kufuatilia bila
kusubiri kuletewa taarifa ofisini ambapo amewapongeza Shirika la Nyumba la
Taifa NHC kwa kufanya Kazi Usiku na Mchana kwa lengo la kuhakikisha ujenzi huo
unakamilika ndani ya Miezi mitatu kama ilivyo Matarajio ya Rais Dkt. John
Magufuli.
Katika ziara hiyo RC Makonda
amemuelekeza Mstahiki Meya wa Ilala Bw. Omary Kumbilamoto kuja na Mpango wa
kuhakikisha miundombinu ya Reli inaunganishwa kwenye machinjio hayo ili Treni
iweze kutumika kupokea wanyama na kusafirisha nyama ndani na Nje ya Nchi.
Aidha RC Makonda amemuelekeza
Meya huyo kuhakikisha ujenzi wa Barabara ya Vingunguti unaanza Mara moja huku
akiitaka Manispaa ya Ilala kufikiria uwezekano wa kulipa fidia kwa wakazi
wanaozunguka machinjio hiyo ili kwa miaka ijayo machinjio iweze kupanuliwa na
kuwa kubwa zaidi.
Pamoja na hayo RC Makonda
amesema kuwa tayari mchakato wa kuagiza mashine mbili za kisasa za Kuchinja na
kuchakata nyama umekamilika ambapo Mashine itakuwa na uwezo wa kuchinja, kusafisha na kuchakata Wanyama
2,000 kwa siku moja.
Katika hatua nyingine RC
Makonda amefanya ziara ya kustukiza kwenye Mradi wa Ujenzi wa Soko la Kisasa la
Kisutu na kumuagiza Mkandarasi wa ujenzi wa Soko hilo kufanya kazi usiku na
mchana ili kuhakikisha ujenzi unakamilika na kukabidhiwa kabla ya mwezi May
Mwakani.
Hatua hiyo imekuja baada ya RC
Makonda kutoridhishwa kasi ya ujenzi wa soko hilo ambalo limekuwa likisuasua
mara kwa Mara huku wataalamu wakitoa taarifa za wongo kuwa ujenzi unaenda
vizuri.
0 comments:
Post a Comment