Thursday, May 6, 2021
WAKAZI WA MKOA WA KATAVI WAIPOKEA BENKI YA NBC KWA SHANGWE
Tuesday, May 4, 2021
Waziri Ndugulile:Tunaandaa sheria ya faragha kulinda taarifa za mtumiaji
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, TEHAMA Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mdahalo wa wadau wa sekta ya Tehama
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Faustine Ndugulile amesema katika kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi ya sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA, anakusudia kutunga sheria ya faragha.
Pia ametoa wito kwa wadau kupeleka mawazo, maoni au ushauri namna ya kuboresha sekta hiyo nchini.
Ndugulile ametoa kauli hiyo juzi katika mdahalo wa wadau wa sekta ya Tehama ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kujadili changamoto na suluhisho kuhusu sekta ya Mawasiliano na tekbnolojia nchini.
Akizungumza katika mdahalo huo uliokuwa na mada kuu kuhusu mapinduzi ya nne ya viwanda kwa uchumi wa dijitali wa ushindani, Dk. Ndugulile alisema wizara yake inakwenda kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali za sekta hiyo.
"Tunaenda kupitia sheria na kanuni zetu na tutafanya mabadiliko ili kukidhi mazingira ya sasa, tunakusudia kutunga sheria ya faragha na kulinda taarifa za mtumiaji(Data Privacy and Protection).
"Nimekuwa msikilizaji wa mdahalo kwa kweli tumepata mengi kutoka kwa wadau na kama serikali tunaenda kuyafanyia kazi kwa haraka.
"Muda wowote wadau leteni mawazo, maoni na ushauri ni namna gani tuboreshe na tusonge mbele uzuri hata mitandaoni nipo ukienda Twitter utanipata, Instagram nipo na twitter nipo na uzuri kwa sasa inapatikana vizuri na mnaipata vizuri pia.
"Kuhusu TCRA nimetoa maelekezo tayari wasifanye kazi kama polisi bali kama mlezi, mimi sio muumini wa faini kubwa kubwa lazima tubadilike na tumeanza kubadilika, alisema.
Akizungumza kwenye mkutano huo Dk Bello Moussa, Mkuu wa Ubunifu na Mikakati ya TEHAMA Huawei Kusini mwa Afrika alisema: "Mapinduzi ya Nne ya Viwanda yanakuja na maendeleo ya kiteknolojia yanaendesha maendeleo ya ulimwengu, ni wakati mzuri sasa kwa Tanzania kutosalia nyuma, bali kuungana na ulimwengu wote kwa kufanya kazi kwenye maeneo ambayo yataharakisha Mapinduzi ya Nne ya Viwanda Tanzania katika Miaka 5 ijayo ”
Alitaja maeneo hayo ambayo ni pamoja na mpango wa kitaifa wa TEHAMA kwa uchumi wa kidigiti, mkongo wa taifa wenye kasi zaidi, ufikiwaji wa huduma ya internet maeneo ya vijijini na wataalamu wa wataalam wa TEHAMA.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga alisema Tehama imeleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali ikiwamo kupunguza gharama za uzalishaji, kuongezeka uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Thursday, April 29, 2021
Hivi ndivyo TEHAMA inaweza kupunguza uzalishaji wa kaboni na kuifikishaAfrika katika uchumi wa kijani.
(Johannesburg, 21 Aprili 2021) Kampuni ya teknolojia ya kimataifa, Huawei inaamini kuwa teknolojia ya habari na mawasiliano au TEHAMA, ina uwezo wa kupunguza uzalishaji wa kaboni ulimwenguni kwa asilimia 20 katika muongo mmoja ujao.
William Xu, ni Mkurugenzi wa Bodi na Rais wa Taasisi ya Utafiti wa Mikakati wa Huawei, hivi karibuni alisema uendelevu wa nishati ni changamoto kubwa ambayo itazikabili nchi zote kwa muongo mmoja ujao.
“Matumizi ya nishati ulimwenguni yanaongezeka kwa kiwango cha asilimia 1.7 kila mwaka. Hivi sasa asilimia 85 ya nishati hutokana mabaki ya mimea na wanyama wa kihistoria yaani ”fossils”. Uendelevu wa nishati hii ni changamoto kubwa inayotukabili sisi sote. Kwa kuwezesha sekta mbalimbali, teknolojia ya TEHAMA ina uwezo wa kupunguza uzalishaji wa kaboni ulimwenguni kwa asilimia 20 katika muongo mmoja ujao." Xu alisema.
Aliongeza kuwa wakati nchi nyingi zimejikita kupunguza uzalishaji wa kaboni, mahitaji ya nishati mbadala yameongezeka, na hapa ndipo TEHAMA inapotoa fursa mpya katika uzalishaji, uhifadhi na matumizi ya umeme.
"Kwa matumizi ya nishati, lazima tupendekeze mifumo jumuishi ya nishati kwa majumbani na viwandani na kuunda jamii, vyuo na miji isiyozalisha kaboni.” alisema Xu.
Hivi karibuni, Huawei ilitangaza kuwa itazingatia ubunifu na teknolojia mpya kusaidia viwanda kupunguza matumizi yao ya nishati ili kupunguza uzalishaji wa kaboni ulimwenguni.
Barani Afrika pia, nchi nyingi zinazidi kuhamia katika matumizi ya nishati mbadala ili kusonga mbele katika nishati endelevu kwa siku zijazo.
Pamoja na algorithm yake ya muunganisho wa gridi inayoendeshwa na utashi wa kutengenezwa (Artificial Intelligence), Huawei imetoa zaidi ya mifano ya gridi 200 ya umeme kwa nchi zaidi ya 30. Hii imesaidia mitambo ya umeme kuunganishwa na gridi kwa uimara huku ikipelekea kuwepo na chanzo bora cha umeme wa jua.
Katika umeme wa jua pekee, Afrika imepata maendeleo makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Zaidi ya gridi 6,200 ambazo hujumuisha gridi kubwa kabisa, za biashara na viwanda pamoja na zile ndogo zimethibitishwa kuwepo barani humo.
Kwa kuongezea, mataifa mengine tisa ya Kiafrika, mbali na Afrika Kusini na Misri, yapo njiani kujiunga na 'Gigawatt Club', lebo isiyo rasmi kwa kundi la nchi zilizo na uwezo wa kuzalisha gigawatt moja ya umeme kutokana na jua.
Huang Su, Mkurugenzi wa Huawei katika Biashara ya Umeme Dijitali Kusini mwa Africa, alisema kwamba karibu nusu ya idadi ya watu wasio na uwezo wa kupata umeme duniani wanaishi kusini mwa jangwa la Sahara.
"Kwa hivyo kuna haja kubwa na ya dharura ya kuharakisha ukuaji wa nishati mbadala kote katika eneo hilo ili kuhakikisha nishati ya kutosha, nafuu na ya kuaminika kwa Waafrika wote na kwa nchi kupata faida ya uchumi wa kijani." anasema.
Huawei imetumia zaidi ya miaka 30 ya utaalam na uzoefu katika teknolojia ya kidijitali ili kufanya uzalishaji wa umeme wa jua na matumizi kuwa bora zaidi na ya kuaminika kwa gharama ndogo.
Sunday, April 25, 2021
Uongozi wa juu wa Benki ya DCB washuhudia mheshimiwa Rais Samia akihutubia bunge kwa mara ya kwanza mjini Dodoma wiki hii


Monday, April 19, 2021
Benki ya Absa yatoa msaada wa wheelchairs 20 kwa wanafunzi wenye ulemavu
HUAWEI YABORESHA UWEKEZAJI ILI KULINDA BIASHARA YAKE
Mwenyekiti wa kampuni ya Huawei Bw Eric Xu
Kampuni ya mawasiliano ya Huawei imebainisha mkakati wake wa kuboresha akaunti yake ya uwekezaji ili kukuza uthabiti na kukabiliana na hali ya mashaka katika biashara inayoletwa na mvutano wa kijiografia, kuibuka tena kwa virusi vya COVID-19 pamoja na kuzuiwa kufanya biashara Marekani.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo Bw Eric Xu, wakati akiwasilisha hotuba kuu katika Mkutano wa 18 wa Wachambuzi wa kidunia. Zaidi ya watu 400, ukijumuisha wachambuzi wa tasnia na wa kifedha, viongozi wa maoni na wawakilishi wa vyombo vya habari walishiriki katika mkutano huo wa siku 3 ulioanza liyoanza Aprili 12 hadi 14, kauli mbiu ikiwa "Ujenzi wa Ulimwengu Wa Maarifa na Uliounganishwa Kikamilifu."
“Uthibiti wa kibiashara ndio kanuni inayotuongoza. Tunataka kuongeza uimara wa biashara yetu yote, na tangu mwaka jana tumekuwa tukifanya kazi kuboresha uwekezaji letu tukiwa na lengo hili akilini.” alisema Eric Xu.
Ripoti ya mwaka 2020 ya Huawei inaonyesha mapato yaliotokana na mauzo ya kampuni hiyo mnamo 2020 yanafika CNY891.4 bilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 3.8 kulinganisha na mwaka uliopita, huku faida yake kamili ilifikia CNY64.6 bilioni, ambayo ukilinganisha na ripoti ya mwaka 2019 ni ukuaji wa asilimia 3.2.
Eric Xu alisema moja ya vipaumbele ni kuongeza zaidi uwezo wa uhandisi wa programu za Huawei. "Tunatafuta fursa mpya za kibiashara katika sekta ya programu. Tunapopata kitu kinachotufaa, tutaongeza uwekezaji ili kuongeza ushiriki wa huduma za program katika vyanzo vyetu vya mapato. "alisema Eric Xu.
Mwisho wa Novemba 2018, Huawei iliamua kuwekeza kiasi cha dola za kimarekani bilioni 2 katika kuboresha uwezo wao wa uhandisi wa programu. Eric Xu alisema kampuni hiyo "inafurahishwa na matokeo hadi sasa".
Programu kwa ajili ya magari kujiendesha ni mojawapo ya malengo makuu ya uwekezaji ndani ya kampuni. Kulingana na Eric Xu, programu hiyo ipo mbioni kufikia hatua ambapo magari yatajiendesha yenyewe bila dereva kujishughulisha kwa namna yoyote ile.
"Pamoja na uwekezaji mkubwa, matumaini yetu ni kusukuma mwenendo huu mbele kwani program hizi zinawezesha ujumuishaji wa tasnia ya magari na ICT, ambayo nayo hutengeneza fursa za kimkakati za muda mrefu kwa Huawei. Mara baada ya ukamilifu wa program hiyo, kutakua na mabadiliko katika sekta zote zilizo karibu ambayo yataleta mabadiliko makubwa zaidi katika miaka 10 ijayo.” Alisema Mwenyekiti huyo.
BENKI YA EXIM YAPANIA KUNUFAISHA WATEJA WAKE HUDUMA ZA KIDIGITAL
Benki Ya Exim Yajizatiti na 'Mteja Kwanza' Utoaji Huduma Za Kidigitali.
Dar es Salaam: Aprili 18, 2021: Benki ya Exim imesisitiza kuhusu mkakati wake wa kuwekeza na kutanguliza zaidi maslahi ya wateja wake hususani katika mipango yake muhimu ikiwemo ile ya uvumbuzi na utoaji wa huduma kwa wateja.
Akizungumza kuhusiana na mkakati huo jijini Dar es Salaam mwishoni nwa wiki, Ofisa Mtandaji Mkuu wa Benki hiyo Bw Jaffari Matundu alisisitiza kuwa benki hiyo imejizatiti kuhakikisha kwamba wateja wake wananufaika zaidi na ukuaji wa technolojia katika utoaji wa huduma za kibenki.
"Lengo ni kuhakikisha kwamba benki ya Exim tunatumia vyema huu ukuaji wa kidigitali katika utoaji wa huduma za kibenki kwa wateja wetu…lengo ni kuona wanaridhishwa na huduma zetu na wanazifurahia. Tunaamini kwamba furaha na ukuaji wao ndio biashara yetu,'' alisema.
Aliongeza kuwa agenda ya uvumbuzi imebaki kuwa kipaumbele cha benki hiyo katika kuelekea kwenye lengo lake la msingi ambalo ni kuifanya benki hiyo kuwa ya kidigitali zaidi huku kipaumbele kikibaki kuwa ni 'mteja kwanza'.
Katika kabiliana na changamoto ya COVID 19 benki hiyo mapema mwaka jana ilizindua kampeni ya "Maliza Kirahisi Kidigitali' iliyodumu katika kipindi cha mwaka mmoja ikilenga kubadilisha tabia ya wateja na kuongeza kasi ya mabadiliko yanayoendelea ya nchi kutoka katika kutumia pesa taslimu kwenda malipo ya dijiti.
"Kampeni hiyo pia inakwenda sambamba na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya kidigitali katika kufanya miamala uchumi pamoja na kuhakikisha wateja wetu wanahudumiwa bila kwenda kwenye matawi" aliongezea.
Ili kurahisisha zaidi miamala na kuifanya bora zaidi na rahisi kwa wateja, benki ina chaguzi kadhaa za huduma kupitia simu na kidigitali ambazo wateja wanaweza kuzitumia kupata huduma na kufanya miamala muda wowowte katika siku saba za wiki Katika kuhakikisha kwamba huduma za benki hiyo zinakuwa jumuishi, huduma ya USSD ndio ilihusika katika kuipamba kampeni hiyo.
''Kila mwingiliano na mteja ni nafasi kwetu kuwaelewa vizuri wateja wetu na namna ya kuwahudimia kulingana na mahitaji yao. Tunapoendelea kupanua huduma zetu, tunaweza kuona jinsi kila huduma inatimiza mahitaji ya watumiaji. Ni suala la kuendelea kujifunza na uvumbuzi. ’
"Zaidi, kusikiliza kwa karibu maoni ya wateja hutusaidia kupata mrejesho unaotuwezesha kufanya maboresho na uvumbuzi ili kuimarisha huduma tunazowapatia. Lengo ni kufanya maisha yao yawe rahisi. Tunazingatia urahisi wa matumizi, na kufanya huduma zetu kuwa thabiti, salama, na haraka.'' alisema.
Sunday, April 18, 2021
NBC YAUNGA MKONO SERIKALI SEKTA YA ELIMU YATOA MSAA VIFAA VYA ELIMU KIBITI
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Bw Gullamhussein Kifu (watatukushoto) akipokea msaada wa madawati viti pamoja na meza 500 kwa ajili ya shule za wilaya hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Wateja wa wadogo wa Benki ya NBC Bw Elibariki Masuke(wa pili kulia) msaada huo ukilenga kuboresha sekta ya elimu Wengine pichani ni Mbunge wa jimbo la Kibiti Bw Twaha Mpembenwe (kushoto),Mkurugenzi wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya NBC Bi Neema Singo (wa pili kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kibiti Bw Abduljabir Marombwa hafla hiyo imefanyika hivi karibuni wilayani kibiti.
Kibiti, Pwani: April 17, 2021: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa msaada wa madawati 250, viti viti pamoja na meza 250 wilayani Kibiti mkoni Pwani ikiwa ni sehemu ya Mpango wa kipekee wa uwajibikaji wa Jamii (CSR) ambao unaplenga kuchangia utoaji wa elimu bora nchini.
Zaidi, benki hiyo pia imetoa mafunzo ya kibiashara na ujasiriamali kwa wanawake wajasiriamali 150 wilayani humo ili kuwajengea uwezo wa kuemdesha biashara zao kwa ufanisi huku wakizingatia nidhamu ya fedha kabla hawajapatiwa mikopokwa ajili ya kukuza mitaji yao.
Madawati hayo yalikabidhiwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo wa benki hiyo Bw Elibariki Masuke wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya Hiyo Bw Gullamhussein Kifu . Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mbunge wa jimbo la Kibiti Bw Twaha Mpembenwe pamoja na maafisa wengine wa wilaya hiyo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji.
Bwana Masuke alisema kuwa benki hiyo imejitolea kusaidia katika kuboresha ustawi wa jamii kupitia misaada ya kijamii ikiwemo elimu na kwamba wameguswa sana na suala la changamoto ya madawatikwenye baadhi ya maeneo hapa nchini sababu iliyosababisha wao kuchukua hatua hiyo ili kuboresha zaidi sekta hiyomuhimu.
"Ni furaha kwetu kuwa sehemu ya kutatua changamoto kwenye sekta muhimu kama hii. Kupitia ushirikiano na ushawishi tunaoupata kutoka kwa Mbunge wa Kibiti na ofisi ya Mkuu wa wilaya tunaahidi kuendelea kushirikiana na jamii ya wana Kibiti huku pia tukifikiria namna kufungua tawi letu wilayani Kibiti kufuatia fursa mbalimbali tunazoziona ikiwemo kilimo na mradi wa kituo cha kupozea umeme wa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere,’’ alisema.
Alishauri pia wanafunzi na walimu watakaonufaika na msaada huo kutunza madawati na meza hizo ili viweze kutumika kwa muda mrefu na hivyo kusaidia walengwa wengi zaidi.
Kuhusu mafunzo kwa wajasiriamali wanawake Bwana Masuke alisema kuwa miongoni mwa sababu zinazokwamisha utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali wengi ni pamoja na wao kuendesha biashara zao bila kuzingatia misingi ya kifedha ikiwemo kutunza kumbukumbu za mahesabu ikiwemo mapato na matumizi.
Kwa mujibu wa Bw Masuke ni kutokana na uwepo wa changamoto hiyo ndio sababu benki hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi nyingine ikiwemo TanTrade, SIDO, VETA na washauri binafsi kuelimisha wajasiriamali kuhusu namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara zao ili kuwajengea uwezo kabla ya kuwapatia mikopo.
"Tumekuwa tukishirikiana na washirika wengine kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwenye maeneo kama usimamizi wa hesabu, utunzaji wa vitabu na uongozi, ili tuwaweke vizuri kwa ufikiaji rahisi wa mikopo", Masuke alisema.
Akizungumza mara tu baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Bw Gullamhussein Kifu pamoja na kuishukuru benki ya NBC kwa kutoa msaada kwa wakati haswa unaohitajika, aliiomba benki hiyo ifungue tawi lake wilayani humo mapema iwezeknavyo ili iweze kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara husani wadogo.
"Msaada huu utasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati katika baadhi ya shule zetu…tunashukuru sana NBC tunaomba muendelee kusaidia kwenye maeneo mengine pia ikiwemo sekta ya afya ." Alisema.
Akizungumzia mafunzo kwa wajasiriamali wanawake wilayani humo Bw Kifu alitoa wito kwa washiriki kuhakikisha wanayatumia vyema kwa kuwa yanalenga kuwasaidia katika upatikanaji wa mikopo sambamba na kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kwa faida
“Kibiti ni wilaya changa inayohitaji watu wake ili kuendelea. Kabla hatujapokea wawekezaji kutoka nje ni lazima tuanze sisi wenyewe humu ndani. Kupitia mafunzo haya tunakwenda kupata wajasiriamali na wafanyabaishara wenye weledi wa kutosha kutambua fursa zilizopo na kuzitumia,’’ alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo hilo Bw Twaha Mpembenwe aliiomba benki hiyo iendelee kuwekeza zaidi wilayani humo kwa kufungua tawi lake sambamba na kuwasaidia wajasiriamali na wakulima hususani wa zao la ufuta pamoja na vijana ambao kwasasa wanakibiliwa na changamoto ya huduma za kifedhaikiwemo mikopo na elimu ya biashara na kilimo cha kisasa.
Thursday, April 15, 2021
TADB na NBC kuwawezesha maelfu ya wakulima kupata mikopo nafuu
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Taifa ya Biashara NBC Elvis Ndunguru (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutia saini mikataba kwaajili kuingia makubaliano yakufanya kazi pamoja na Benki ya Taifa ya Biashara NBC yenyelengo la kuwawezesha maelfu ya wakulima wadogo katika minyororo ya thamani ya kilimo wengine pichani kulia ni maofisa wa Benki ya TADB.
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Taifa ya Biashara NBC ElvisNdunguru (kulia), akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla yakuingia makubaliano yakufanya kazi pamoja na Benki ya Maendeleo ya kilimo TADB yenyelengo la kuwawezesha maelfu ya wakulima wadogo katika minyororo ya thamani ya kilimo kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB, Derick Lugemala.
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Taifa ya Biashara NBC ElvisNdunguru wapili (kushoto waliokaa) pamoja na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB, Derick Lugemala wakitia saini Mkataba wa makubaliano wa kufanya kazi pamoja kwaajili ya kuwawezesha wakulima wadogo katika minyororo ya dhamani ya kilimo wanaoshuhudia kulia ni Meneja wa Mfuko maalum wa dhamana kwa wakulima wadodo kutoka TADB Asha Tarimo pamoja na Mkurugenzi wa sheria wa TADB Edson Rwechungura Picha na Brian Peter

TADB na NBC kuwawezesha maelfu ya wakulima kupata mikopo nafuu
· Zadhamiria kukuza mitaji na kuleta mageuzi katika kilimo, uvuvi na ufugaji
Dar es Salaam. Jumanne, 13 April, 2021. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia katika makubaliano na benki ya biashara NBC kuwawezesha maelfu ya wakulima wadogo wadogo nchini kupata mikopo yenye riba nafuu ili kuweza kukuza biashara zao na kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
Makubaliano haya, yaliyosainiwa leo katika makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam, yataiwezesha benki hiyo kutoa dhamana kwa wakulima watakaoenda kuomba mikopo NBC kufanya shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi kwa riba nafuu ya asilimia kumi na nne (14%) tu. Dhamana hii inaratibiwa na TADB chini ya mfuko maalum wa dhamana kwa wakulima wadogo nchini ‘SCGS’.
“Kwa muda mrefu tumeona wakulima wetu nchini wakipata changamoto ya mitaji. Wengi wakilazimika kukopa kwa riba za kibiashara ambapo wengi wao wamekuwa wakipata changamoto ya kuhimili riba hizo kubwa. Hivyo, kama taasisi ya maendeleo ya kifedha, kupitia mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo, tumeona umuhimu wa kutoa mikopo hii nafuu kwa kushirikiana na NBC ili kuwawezesha wakulima wengi zaidi kupata mitaji,” alieleza Derick Lugemala, Mkurugenzi wa Fedha kutoka TADB.
Kwa upande wake, Elvis Ndunguru, Mkuu wa Biashara za Kibenki kutoka NBC, alisema kwamba mikopo hiyo watakayokuwa wanatoa kwa dhamana ya TADB itawawezesha kuwakopesha wakulima wadogo mikopo ya mtaji hadi kiwango cha shilingi 50 milioni kwa mkulima mmoja mmoja, shilingi 500 milioni kwa vikundi na vyama vya wakulima, na hadi shilingi 1 bilioni kwa kampuni ambazo miradi yake inawaunganisha na kuwanufaisha wakulima wadogo wengi.
Akieleza vigezo vya kupata mikopo hiyo, Ndunguru alisema:
“Ili kukidhi vigezo vya kupata mikopo hii, mkulima anahitajika kuwa amefanya biashara ya kilimo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu, awe na leseni ya biashara. Awe na kumbukumbu ya taarifa za kifedha. Mikopo hii inapatikana katika matawi yote ya arobaini na saba (47) ya NBC yaliyopo Tanzania bara na Zanzibar. Tunatoa rai kwa wakulima wote wadogo kuchangamkia fursa hii.”
Hapo awali, Lugemala alisema, lengo la mikopo hii yenye masharti nafuu ni kuchagiza benki za kibiashara na taasisi za kifedha kutoa mikopo zaidi kwa wakulima na kuwezesha ukuaji wa minyororo yote ya thamani yanayohusiana na kilimo, uvuvi na ufugaji nchini.
“Mpaka Desemba 2020, mfuko huu wa dhamana ulikwisha toa mikopo katika miradi ya kilimo, uvuvi na ufugaji yenye thamani ya shilingi bilioni 66 na kuwafikia wanufaikaji zaidi ya 9000 moja kwa moja na wasionufaika moja kwa moja 750,000. Baadhi ya miradi tuliyowezesha ni pamoja na kwenye korosho, mpunga, kahawa, miwa, mahindi, mihogo, pamba na ufugaji wa kuku,” alifafanua Lugemala.
Kutokana na taarifa kutoka TADB, mfuko huu wa dhamana ulianzishwa Februari 2018. Na katika kipindi cha miaka mitatu sasa, TADB imeshashirikiana na benki na taasisi za kifedha kama NMB, CRDB, Azania, Benki ya Posta (TPB), Stanbic, FINCA Microfinance, UCHUMI Commercial Bank, Tandahimba Community Bank (TACOBA), Mufindi Community Bank (MUCOBA) na NBC.
“TADB inaamini kwamba kupitia mtandao huu wa ushirikiano wa kimkakati, idadi kubwa ya wakulima wadogo watafikiwa na kuwezeshwa,” alisisitiza Lugemala.
xxxx Mwisho xxxx
Kuhusu TADB:
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ni benki ya umma yenye malengo ya kuongoza mikakati ya kujenga uwezo na mipango ya kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo na kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuunda na kutekeleza sera za kilimo na mikopo ya vijijini. Mpaka Desemba 2020, TADB imekwisha nufaisha wakulima 1,788,202 na kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 300 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mikopo hii imewezesha kukua kwa minyororo ya thamani kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kuhusu NBC:
Benki ya NBC ni benki pekee ya kimataifa inayopatikana katika mikoa na maeneo mbalimbali nchini ikiwa na matawi 47 na mashine za ATM zaidi ya 180, pamoja na Mawaka zaidi ya 3,000. Benki ya NBC inatoa huduma mbalimbali za ukusanyaji fedha za huduma nyingine za kibenki kwa wateja mbalimbali kwa zaidi ya miaka 54 nchini . Benki ya NBC sasa imeajiri wafanyakazi takriban 1,100 nchi nzima.
Kwa maelezo zaidi au msaada tupigie +255 76 898 4000/4011 | +255 22 219 3000 | +255 22 551 1000 or email us NBC_Marketingdepartment@nbc.co.tz
Kwa taarifa zaidi:
Amani Nkurlu, Meneja Mahusiano na Masoko – TADB
Barua pepe: amani.nkurlu@tadb.co.tz Simu: +255 754 878 385 au +255 712 223 839
David Raymond, Meneja Mwandamizi-Chapa na Mawasiliano
National Bank of Commerce Limited (NBC)
Barua pepe: david.raymond@nbc.co.tz
Simu: +255 717 742832















