Wadau mbalimbali wanasema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia, hususan akili mnemba (AI), zinachochea uzalishaji wa bidhaa zinazoleta suluhisho na kukidhi matarajio yanayobadilika ya watumiaji, hivyo kufanya uhitaji wa kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia kuwa muhimu kwa kampuni zinazotaka kuendelea kuwa na nafasi katika soko.
Mkurugenzi wa Masoko wa MeTL Group, Fatema Dewji, alisema biashara zitakazoshindwa kuendana na maendeleo ya kiteknolojia zinaweza kuachwa nyuma, kutokana na ubunifu kuendelea kuwa na nafasi kubwa katika uuzaji, usambazaji na uundaji wa bidhaa.
“Wakati maendeleo na mabadiliko ya teknolojia yakiendelea kushika kasi, matumizi yake yanazidi kuchochewa hususani kwenye maeneo ya uzalishaji na endapo kama kuna biashara ambazo haziko tayari kukabiliana na haya mabadiliko, zitaachwa mbali sana,” alisema Fatema kwenye hafla ya mashirikiano baina ya MeTL group na Haier Tanzania yaliyofanyika wikiendi hii.

Ushirikiano huo unakuja wakati ushindani katika soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani ukizidi kutegemea uwezo wa biashara kuunganisha ubunifu wa kiteknolojia na ubora wa bidhaa ili kutimiza mahitaji ya walaji.
Hata hivyo, aligusian juu ya mitazamo ya watu kuhusu AI ambapo wengi wanaitazama kama ni tishio kwenye soko la ajira ambapo alisema licha ya nguvu yake, bado ubunifu na mawazo ya binadamu vitaendelea kuwa muhimu hata wakati biashara zikiongeza matumizi ya teknolojia mpya.
“Teknolojia hii haiwezi kuchukua nafasi ya mawazo au watu wenye ubunifu na fikra,” alisema, akiongeza kuwa inaweza badala yake kuwasaidia wafanyakazi, wakiwemo wanaohusika katika uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Haier-Tanzania, Liu Chi, alisema soko la vifaa vya matumizi ya nyumbani hapa nchini linaendelea kubadilika, ambapo watumiaji wengi sasa wanaangalia zaidi ubora wa bidhaa, hivyo kama kampuni zinawajibu wa kuhakikisha zinazalisha bidhaa zenye tija ili kufikia mahitaji ya walaji.










0 comments:
Post a Comment