
Mwenyekiti wa Shirikisho la kimataifa Kriketi (ICC) Jay Shah katikati uzinduzi wa Uwanja wa kisasa wa chama Cha Kriketi Tanzania (TCA CricketArena) iliyojengwa katika viwanja vya michezo vya chuo kikuu cha Dar es Salaam, ambapo kiwanja hicho kitatumika kama kituo cha taifa cha kukuza vipaji na kuandaa timu za taifa wanaume na wanawake na vijana chini ya miaka 19, wengine pichani ni wadau wa michezo hiyo.

Shirikisho la Kimataifa la Kriketi (ICC) limeeleza kuwa Tanzania ina nafasi ya kuwa miongoni mwa mataifa yatakayoweza kuandaa mashindano makubwa ya kriketi duniani,
kufuatia uzinduzi wa Uwanja wa Kisasa wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA Cricket Arena) uliojengwa katika viwanja vya michezo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uwanja huo utatumika kama kituo cha taifa cha kukuza vipaji na kuandaa timu za taifa za wanaume, wanawake na vijana chini ya miaka 19.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa ICC, Jay Shah, amesema uwekezaji wa Tanzania katika miundombinu ya kisasa na maendeleo ya vijana umeifanya nchi kuwa miongoni mwa mataifa yanayokua kwa kasi katika mchezo wa kriketi barani Afrika. Amesema endapo juhudi hizo zitaendelea, Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi zitakazoandaa Kombe la Dunia la Kriketi siku zijazo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Hamisi Hassan Abdallah, amesema uwanja huo utaongeza uwezo wa Tanzania kuandaa mashindano ya kimataifa na kuwapa wachezaji mazingira bora ya mazoezi yanayokidhi viwango vya kimataifa. Amebainisha kuwa awali chama hicho kilikuwa na uwanja mmoja pekee, hali iliyokuwa ikikwamisha jitihada za kuandaa mashindano makubwa.
Naye Afisa Mwandamizi wa Michezo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (NSC), Apansia Lema, amesema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo ili kukuza vipaji vya vijana. Amesema zaidi ya shule 400 nchini sasa zinashiriki mchezo wa kriketi, huku kufuzu kwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 19 kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2026 kukitajwa kuwa hatua muhimu katika maendeleo ya mchezo huo nchini.











0 comments:
Post a Comment