A blog that gives out financial institutions news on time with accurate informations.


Thursday, April 4, 2024

KAMPUNI ya Gesi ya Oryx Tanzania imeahidi kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za watanzania.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Meja Edward Gowele(wa tatu kushoto) akimkabadhi mtungi wa gesi ya Oryx Furaha Mawikia wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi na majiko yake 400 kwa wanawake wa vijiji vya Mwalusembe ,Kinene,Kitomondo na Kisele wilayani Mkuranga. Wengine pichani ni Balozi wa Heshima Shelisheli nchini Tanzania Maryvyonne Pool(watatu  kulia) Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Janeth Mutashobya (wa kwanza kulia), Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga Omary Mwanga.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele(kulia) pamoja na  Balozi wa Heshima wa Shelisheli nchini Tanzania Maryvyonne wakiangalia vyakula vya asili ya kitanzania ugali,wali na mboga ambazo vimepikwa kwa kutumia jiko la gesi ya Oryx wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi 400 yakiwa na
majiko yake kwa wanawake wa Kata ya Mwalusembe wilayani humo.
Baadhi ya wanawake wa Kata ya Mwalusembe wilayani Mkuranga mkoani Pwani wakiendelea kupika chakula kwa kutumia jiko la Oryx wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi ya Oryx kwa wanawake wa vijiji vya kata ya Mwalusembe wilayani Mkuranga.

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

Hayo yameelezwa na Meneja Usalama Afya na Mazingira wa Oryx Energies Tanzania, Janet Mutashobya, alipomwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Benoite Araman wakati wa hafla ya kugawa mitungi 400 ya gesi na majiko yake kwa akinamama wa Kata ya Mwalusembe wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Ugawaji wa mitungi hiyo umefanyika kwa ushirikiano wa Balozi wa Heshima wa Shelisheli nchini Tanzania Maryvyonne Pool ambaye pia ni Mwanzilishi wa taasisi ya African Reflections Foundation ambayo imekuwa ikijihusisha na kusaidia jamii katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo

"Kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti. Pia ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa," amesema.

Ameongeza kupika kwa kutumia nishati safi kunafungua fursa kwa wanawake kutumia muda mwingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji wa kiuchumi.

"Kwa kuanawake wanatumia muda mchache kupika hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula. Kwa kutumia gesi ya Oryx, Watoto wanakua na muda mwingi zaidi kusoma na sio kwenda kutafuta kuni,"amesema Mutashobya.

Aidha amesema kwa  miaka mingi Oryx Gas imekuwa kampuni kiongozi katika kukuza matumizi ya Gesi nchini Tanzania na Kuanzia Julai  mwaka 2021 wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali waliyopokea toka kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Amesema kupitia mipango hiyo Oryx Gas inataka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa ambayo si tu mbaya kwa afya zetu bali pia ni hatari kwa mazingira yao  na pia Oryx Gas inatekeleza juhudi za kueneza matumizi ya nishati safi kwa Watanzania wengi ipasavyo ambayo ni ndoto kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Balozi Pool amesema  uamuzi wa kushirikiana na Oryx kutoa mitungi hiyo kwa wanawake wa vijiji vya kata vya Mwalusembe, unatokana na kutambua na kuunga mkono jitihada za Rais Samia za kuhamasisha nishati safi ya kupikia.

“Hii kwangu si mara ya kwanza kwani mwaka 2022 nilinunua mitungi ya gesi na kugawa kwa wanawake wa Mkuranga kwa sababu mimi ni balozi wa heshima hapa Mkuranga. Ndio maana nimekuwa nikishiriki katika miradi ya maendeleo ukiwemo wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji,” amefafanua.

Ameeleza taasisi yake imekuwa ikiwasidia wanawake na vijana kulima, huku akibainisha kuwa hatua hiyo ya kusaidia wanawake hao kupata nishati safi ya kupikia imetokana na kutambua mchango wa Rais Dk. Samia baada ya kuwa champion wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

"Kulifanyika mkutano wa mazingira wa kimataifa Dubai ambapo Rais Samia alichaguliwa kuwa champion wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia , hivyo ni vema kumuunga mkono Rais Samia katika ajenda hiyo.

“Katika ule mkutano nilikaa meza moja na Rais (Dk.Samia) pamoja na Bilionea wa Marekani Bill Gate ambapo Rais Samia alichaguliwa kuwa champion wa Afrika katika kuhamasisha nishati safi, hivyo anastahili pongezi na nimeahidi kuunga mkono na kumsaidia kadri nitakavyoweza,”amesema Balozi Pool.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Rufiji ambaye pia anakaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Meja Edward Giwele, amesema umefika wakati wa kumuunga mkono kwa vitendo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuokoa mazingira na kutanua fursa za kiuchumi hususan kwa wanawake wa wilaya hiyo nan a maeneo mengine nchini.

"Tumegawa mitungi ya gesi 400 kwa wanawake wa kijiji cha Kinene katika kata ya Mwalusembe ndani ya wilaya Mkuranga ikiwa sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha tunatumia nishati safi au nishati mbadala na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa."

Amewapongeza Oryx na Balozi Pool Afrika Reflections Foundation kwa kushirikiana na kuhakikisha wanagwa mitungi hiyo kwa akinamama tena wa hali ya chini kabisa katika kijiji hiki cha Kinene.

Awali KatibuTawala Wilaya ya Mkuranga Omar Mwanga, amesema Wilaya  hiyo ni miongoni mwa wahanga wa uharibifu wa mazingira kwani misitu mingi ya asili imekatwa mkaa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuwivisha chakula.

"Miti inakatwa kwa ajili ya kuchoma mkaa katika maeneo yetu, misitu ya vijiji ambayo imehifadhiwa na mingine ya asili imekuwa ikiathirika na wananchi kufanya shughuli za kijamii hasa zaidi ya hizi shughuli za ukataji mkaa, kwa hiyo na sisi tunaendelea kuhamasisha kama wanavyofanya Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania.
Share:

0 comments:

Post a Comment


Propellerads

Search Brazuka Kibenki

FOLLOW US ON FACEBOOK

  • ()
  • ()
Show more

Labels

Blog Archive